Saturday, 31 May 2014

Loga asajili watano wa timu za taifa


Kocha Zdravko Logarusic.

KOCHA Zdravko Logarusic amesema anataka Simba kusajili wachezaji watano wa kimataifa ambao watakuwa wanacheza kwenye timu za taifa na si vinginevyo.
Akizungumza kutokea katika mji ulio kilomita 400 kutoka Jiji la Zagreb, Croatia, Loga aliliambia Championi Ijumaa kuwa, wachezaji watano wa kulipwa wa Simba, kila mmoja anapaswa kuwa katika kikosi cha timu yake ya taifa.
“Lengo la Simba ni kufanya vizuri na kama utasajili wachezaji kutoka nje, lazima kila mmoja awe kwenye kikosi cha timu yake ya taifa.
“Sitaki mchezaji ambaye atakuja Simba halafu akae kwenye benchi, nimeamua kufanya hivi ili kuwa na wachezaji wa kimataifa ambao ni msaada,” alisema.
Logarusic ambaye yupo mapumzikoni nyumbani kwao Croatia, amesisitiza kwamba kama Simba itasajili wachezaji kutoka Tanzania, lazima wawe majembe.
Hata hivyo, taarifa nyingine zinaeleza kuwa katika ripoti yake ya nusu msimu uliopita, alisisitiza wachezaji watatu wa kimataifa wabaki.
Aliwataja anaotaka wabaki kuwa ni Donald Musoti, Joseph Owino na Amissi Tambwe ambaye ameibuka kuwa mfungaji bora wa Ligi Kuu Bara.
Hivyo, Loga atakuwa na kazi ya kusaka wachezaji wawili tu kutoka nje ya Tanzania ili kutimiza idadi ya watano kwa mujibu wa kanuni za TFF.
Hata hivyo, uhakika wa kocha huyo kurejea Simba ni baada ya uchaguzi na tayari Zacharia Hanspope ambaye ni mwenyekiti wa kamati ya usajili alimpa dola 8,000 (zaidi ya Sh milioni 13) ili aweze kuamini kwamba klabu hiyo inamhitaji kweli.

No comments:

Post a Comment